Bonta azungumzia sababu za matokeo mabovu kidato cha nne

Rapper wa Nauza Kura Yangu, Bonta amekuwa msanii mwingine wa Hip Hop nchini kutoa sauti yake kufuatia matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana. Amesema matokeo ya kidato cha nne mwaka huu ni mabovu kwakuwa serikali imechagua kuwa na shule nyingi badala ya kuzingatia ubora wa elimu.

 

“Serikali yetu imechagua mfumo wa quantitative education na sio qualitative, yaani wanazingatia zaidi kuwa na shule nyingi ambayo ndi quantity lakini hawaangalii quality za hizo shule, ni sawa sawa na kuchukua sukari kijiko kimoja ukajaza chai katika pipa halafu ukakoroga ile sukari,” anasema Bonta.

 

Amesema ubora wa elimu yetu imekuwa ndogo ukilinganisha na wanafunzi wanaomaliza ambao ni wengi.

“Hiyo namba asilimia kuwa ya waliofeli inaonekana kubwa kwasababu watu wametoka wengi katika shule za kata. Huwezi ukamfananisha mwanafunzi anayesoma Feza Boys pale na mwanafunzi ambaye anasoma labda shule ya kata ya Isaka, sababu kule unakuta wana walimu zaidi ya ishirini, hapa kuna walimu wanne, walimu wanne hao kwa mwezi wa siku 30 wanaweza wakafundisa hata siku 20 maake kuna weekend, mwalimu huyu kafuata mshahara mjini mbali atakaa siku mbili tatu atarudi, hakuna maabara, hakuna vitabu,”

 

Bonta ameongeza kuwa miaka ya hivi karibuni elimu imekuwa ghali na hivyo kugeuka kuwa kama bidhaa.

“Elimu imekuwa ni commodity, elimu imekuwa ni bidhaa kama sukari, mtu mwenye hela ndio anakunywa chai yenye sukari, mtu ambaye hana sukari anakunywa chai ambayo haina sukari, ada imekuwa kubwa kiasi kwamba mtu unalipa ada utadhani unataka kununua shule. Utagundua kuwa wanaosoma ni matajiri, maskini sisi tunafuta ujinga tu,” anasema Bonta.