Kampuni ya Onmobile ya India yazuiwa kufanya kazi kutokana na kuibia wasanii wa Tanzania

 

Serikali imeizua kampuni ya Onmobile ya India kuendelea na biashara ya kuuza kazi za wasanii wa Tanzania kinyemela.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la alhamis hii July 26, kampuni hiyo ya kigeni imekuwa ikifanya kazi nchini kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kampuni hiyo imekuwa ikivuna mabilioni ya fedha kutokana na jasho la wasanii wa muziki, wengi wakiwa ni wale wa muziki wa ‘kizazi kipya’.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo ulibaini kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na kampuni za Airtel na Vodacom na kwa mwaka hutengeza faida ya takriban bilioni Sh23 kutokana na biashara ya kuuza nyimbo za wasanii kwa wateja wa mitandao hiyo (collar tones).

Nyimbo hizo ni zile ambazo mteja wa mtandao husika, huomba ili akipigiwa simu asikie wimbo huo na huduma hiyo hutozwa Sh300 kwa kila wimbo.

Uchunguzi ulibaini kuwa, kila siku Kampuni ya Airtel hupata Sh15 milioni huku Vodacom wakipata karibu Sh20 milioni kutokana na bishara hiyo.

Jana suala hilo liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye alisema kampuni za simu zimekuwa zikiwanyonya wasanii kupitia milio ya simu.

Akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Zitto alisema licha ya kampuni za simu kutumia nyimbo hizo za wasanii zimekuwa zinawanyonya kwani hawalipwi inavyostahili.

“Kampuni za simu zinaingiza Sh43 bilioni kupitia nyimbo za wasanii, lakini kati ya hizo asilimia 80 ya fedha hizo zinachukuliwa na kampuni hizo huku asilimia 13 zinaenda kwa wakala na msanii anapata asilimia saba tu,” alisema na kuongeza:

“Kibaya zaidi, wakala huyo anayejulikana kwa jina la Onmobile ambaye ameingia mkataba na kampuni kubwa za Vodacom na Airtel hajasajiliwa. Ameajiri watu wawili, lakini anatengeneza mabilioni kupitia jasho la wasanii.”

Zitto alipendekeza kuwa, wakala huyo afukuzwe nchini kwa kuisababishia nchi hasara na kushauri kipato cha wasanii kupitia nyimbo zinazotumika kwenye miito ya simu kiongezwe hadi asilimia 50 ili kuwawezesha kujikimu kimaisha.

“Wasanii wapate haki yao na walipwe kutokana na jasho lao. Kazi ya dola ni kumlinda mnyonge. Kampuni za simu ni giant (kubwa), ukiwauliza wanasema hawana mkataba na wasanii. Kwa nini kampuni hiyo ifanye kazi bila leseni?” alihoji.