Steve Nyerere awekwa lupango baada ya kusababisha ajali

Movie mpya ya Msanii wa kuigiza sauti za Viongozi Steve Nyerere, iliyokuwa ianze kurekodiwa jana imeingia dosari baada ya msanii huyo kupata ajali na kuswekwa lupango katika kituo cha Polisi cha Mabatini, asubuhi  ya jana.

Kwa mujibu wa Blog ya AudifaceJackson, msanii huyo amepata ajali hiyo maeneo ya karibu kabisa na kituo cha Mabatini, wakati akiwa na msafara wa wasanii wenzake wanaoshiriki katika Movie hiyo, wakati wakielekea kuanza kurekodi.

Wasanii hao pamoja na Steve, walikuwa wakitokea katika Kambi yao iliyokuwa maalum kwa maandalizi ya kuanza kurekodi ikiwa ni pamoja na kufanyia mazoezi katika kambi hiyo iliyodumu kwa wiki kadhaa.

Ajali hiyo ilikuwa kama hivi:-

Wakati Steve akiwa na baadhi ya washiriki wa movie yake katika gari lake na wakiwa katika mwendo kuelekea eneo la kushuti scenes zao, ghafla aliona gari aina ya funcargo ikiwa imesimama mbele yake huku katikati ya barabara akiwapo jamaa aliyekuwa akisimamisha magari katika eneo hilo.

Baada ya kushindwa kusimama kwa ghafla ndipo alipoigonga gari hiyo kwa nyuma na gari hiyo kutumbukia mtaroni.

 

Mashuhuda wa ajali hiyo walieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni fundi umeme aliyekuwa akisimamisha magari katika eneo hilo ili kuweza kuondoa waya wa Umeme uliokatika na kulala katikati ya barabara huku ukiwa na moto, ili kuepusha madhara zaidi.

Baada ya ajali hiyo, walifika askari Polisi wakiambatana na askari wa usalama barabarani, ambapo alianza kupima ajali hiyo huku madereva wakijibizana na fundi aliyesimamisha magari, ambapo majibizano hayo yaliingiliwa kati na mmoja kati ya askari waliofika eneo hilo.

 

Katika majibizano hayo baina ya fundi, Askari na madereva wote wawili, ndipo kulitokea kupishana kauli baina ya Steve na Askari huyo, aliyediriki kumuita Steve mjinga, ambapo Steve alishindwa kuvumilia na kuamua kumjibu na ndipo alipokunjwa 'Tanganyika Jeki' na kukokotwa hadi katika gari walilokuja nalo askari hao na kumpakia na kisha kuondoka naye kuelekea katika Kituo cha Mabatini.