Tamasha la ukumbusho wa Vita vya Majimaji Tanzania

Maadhimisho ya Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni Kitaifa yamekuwa yakiadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Februari, Mkoani Ruvuma kuanzia mwaka 2010.  Dhana ya maadhimisho haya ni kufanya  Kumbukizi za Vita ya Majimaji ziwe kichocheo cha mabadiliko kwa jamii kifikra na Kiutamaduni.  Kuwaleta pamoja wadau wa historia ya Vita vya Majimaji. Pia kuwakumbuka Mashujaa  wa Vita vya Maji Maji walionyongwa tarehe 27 Februari,1906 na Wajerumani ambao wamezikwa katika eneo la Makumbusho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji – Songea. Vilevile Kutoa fursa kwa jamii kushiriki katika kuenzi na kuendeleza urithi wetu  kupitia shughuli za kimila zinazofanywa na Wazee  wa Baraza la Mila na desturi za jamii iliyohusika katika tukio la Vita vya Maji Maji. Na kutoa elimu kwa Umma wa Watanzania kwa ujumla kuhusu Kumbukumbu za Kimakumbusho kupitia matukio ya kimila na kihistoria. Kuweka dhahiri madhumuni ya kuanzishwa kwa Makumbusho ya Taifa nchini kwa vitendo.

Katika maadhimisho haya Waziri wa Mali asili na utalii Dkt.Hamis Kagasheki ameitaka jamii nchini kuenzi harakati hizo zilizofanywa na mababu wa taifa hili katika kupinga utawala wakikoloni. Pia amesema amefurahishwa kuona kuwa maadhimisho ya kumbukizi ya vita vya majimaji yamekuwa na historia ya kuadhimishwa mwezi februari Mkoani Ruvuma katika ngazi ya mkoa tangu nchi yetu ipate uhuru, Hii imelenga kuwakumbuka  Mashujaa wa Vita vya Maji Maji. Hii imeonesha kwa jinsi Uongozi wa mkoa , Wazee wa Baraza la Mila na Desturi na wananchi wanavyothamini mchango waliokuwa nao Mashujaa hawa hata kujitoa mhanga kutetea uhuru, haki na utawala wao pamoja na kulinda mila , tamaduni na rasilimali zilizopatikana kwenye maeneo yao kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla. Hili ni jambo la kuigwa na kila mtu kuthamini na kulinda urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijazo.

Akiendelea kusema ameshuhudia kuwepo kwa taarifa za mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Mkomanile ambaye alishiriki katika harakati hizo za mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni hivyo ni ishara kuwa akina mama nao walishiriki kikamilifu katika mapambano hayo dhidi ya ukoloni ambapo kwa upande wa Tanganyika ilikuwa ni Vita ya Maji maji ,na kwa upande wa Kenya ilikuwa ni Mau mau na vyote vilikuwa ni chanzo cha vuguvugu la ukombozi wa bara la Afrika. Pia ametoa wito kwa wadau wa utafiti kufanya utafiti zaidi  habari za mwanamke huyo ili nazo ziweze kuingizwa kwenye historia ya kumbukizi hiyo ya vita ya Maji Maji ambayo pia ilikuwa ni chachu ya ukombozi wa bara la Afrika kwa ujumla.