Utafiti: Wanaume waliooa wanawake wenye mshiko zaidi yao huathirika kisaikolojia wakati wa tendo la ndoa

Source: Gazeti la Mwananchi (Feb, 16)

WANAUME waliooa wanawake wenye mishahara mikubwa au vyeo kuwazidi wao, huathirika kisaikolojia wakati wa tendo la ndoa na wengi wao hutoka nje ya ndoa. Utafiti umebaini.

Utafiti huo uliofanywa katika nchi za Denmark na Marekani umebaini kuwa wanaume wanaopata mshahara mdogo, hawashiriki tendo la ndoa kwa ufanisi na wake zao walio na mishahara mikubwa, ukilinganisha na wanaume walio na kipato kikubwa kuwazidi wake zao.

 

Msaidizi katika utafiti huo Dk Lamar Pierce ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Mipango katika Chuo Kikuu cha Washington alisema kuwa wanaume huwa dhaifu kiutendaji katika tendo la ndoa, inapotokea mwanamke ana cheo au kipato kikubwa kuliko yeye. Hata hivyo, utafiti huo haukuwahusisha wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa.

 

Mtafiti huyo alisema kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika, ambapo mfumodume umetawala huku mapinduzi ya kijinsia yakianza kushika kasi. Dk Pierce alifanya utafiti huo kwa kuchunguza taarifa za sampuli zaidi ya 600,000 za wakazi wa Denmark, ambapo wanandoa wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 49 walichunguzwa, kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.

 

Ilibainika kuwa kwa mabadiliko ya kijamii katika siku za hivi karibuni, wanawake wamekuwa watafutaji wakuu kuliko wanaume, yamevunja tamaduni na wajibu wa mwanamume, hali inayowaathiri kisaiokolojia wanaume.

“Hamu ya tendo la ndoa na ufanisi vinahusiana kwa karibu na kipato, mitandao ya marafiki, cheo na ile hadhi ya mwanamume kuwa kiongozi katika familia,” alisema.

Akizungumzia utafiti huo Dk Kitila Mkumbo, Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa madhara wanayoyapata wanandoa wa aina hiyo yanasababishwa na tamaduni na mfumodume. Alisema mila na desturi zinawafanya wanaume wasijiamini pale wanapochangia kidogo katika familia.“Iwapo mwanamume atamchukulia mke wake kama rafiki na siyo msaidizi wa nyumbani, hawezi kuathirika, tatizo kubwa ni kuwa wanahisi kukosa hadhi ya ‘ubaba’,” alisema Mkumbo.

 

Alisema kwamba wanaume wengi wa aina hiyo hutoka nje ya ndoa zao kuwatafuta wanawake wanyonge zaidi yao, ambapo hupata faraja ya tendo la ndoa. Aliongeza: “Wanaume wengi, ambao wake zao wana hadhi na kipato kikubwa, mara kwa mara huwa na hasira, ukali bila sababu, mambo ambayo husababisha waikose raha ya tendo la ndoa kwa wake zao.”