Wanafunzi wa Kike Watumia Mitandao ya kijamii Kujiuza

Leo hii gazeti la Mwananchi limechapisha habari kuhusu madhara ya utandawazi na jinsi gani siku izi inavyotumika vyuoni na mabinti wengi katika biashara ya ngono. Mitandao iyo ni pamoja na facebook, twitter,instagram na bbm, wamendika;

Baadhi ya wanafunzi hao wanatumia mtandao wa ‘University Tanzania  Jokes’, ‘Jicho la Mvulana Liko Fasta Kuliko Google’, ‘Benki ya Utamu Tanzania’ na nyingine katika kufanikisha biashara hiyo ya ngono.

Wasichana hao walijitambulisha kwa majina, vyuo na vitivo wanavyosoma na baada ya kuwafuatilia kwa kuweka ahadi za kimapenzi ilithibitika kuwa wanafanya biashara ya ukahaba huku wakiwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Mmoja wa wasichana hao alijitambulisha kwa jina la Bianca (sio jina lake halisi), ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baada ya mwandishi kufanya naye mawasiliano walikubaliana kukutana eneo la Udasa na muda wa ahadi ulipofika, mwandishi alifika eneo hilo na kukutana na binti huyo ambaye aliiona picha yake na namba ya simu kwenye mtandao, tofauti na alivyodhani awali kuwa huenda wasichana hao wanatumia picha za watu wengine kujinadi.

Kutokana na lengo la msichana kuwa ni biashara ya ngono, mwandishi wa gazeti hili alilazimika kumpeleka binti huyo katika hoteli moja maarufu jijini, akimweleza kuwa inabidi wanywe pombe kwanza kabla ya kwenda chumbani kwa makubaliano ya kumlipa Sh50,000.

Binti huyo alikabidhiwa fedha hizo ili kumwaminisha uhalisia wa kuwapo hitaji na muda wa kwenda naye chumbani ulipofika waliongozana lakini mwandishi akatoroka  njiani akiwa amethibitisha kuwapo kwa tabia hiyo.

Gazeti hili lilimfuatilia mwanafunzi mwingine ambaye alijitambulisha kuwa anasoma katika Chuo cha Ustawi wa Jamii, ambaye kama ilivyokuwa kwa wa kwanza, hakupata taabu kujieleza.

Baada ya mwandishi kueleza alipoipata namba yake mazungumzo yao yalikuwa hivi:
Binti aliuliza: “...Kwa hiyo, uko wapi?”
Mwandishi alijibu:  “Nipo Ubungo.”
Binti akauliza tena: “Unaweza kuja Ustawi?”

Baada ya mawasiliano hayo mwandishi aliambiwa binti huyo kuwa anaweza kumfuata chuoni hapo.

Mwandishi wa gazeti hili alifika maeneo ya Kijitonyama jirani na kilipo chuo hicho, na kumpigia simu binti huyo, ambaye aliipokea na safari hii alimwambia mwandishi kuwa ikiwezekana aje na rafiki yake.

Ilichukua nusu saa kwa wasichana hao kufika katika baa, ambayo mwandishi alikaa kuwasubiri, mara walitokea wasichana hao wakiwa wachangamfu, warembo waliovalia mavazi ya kisasa, yaliyoacha sehemu kubwa ya miili yao wazi.

Muda wa dakika saba walizokaa zilitosha kuwafanya wazoeane na mwandishi kama vile waliwahi kukutana miaka mingi ya nyuma, stori, vinywaji na mambo yalifanyika  kama ilivyokuwa Udasa.

Mwananchi Jumapili liliendelea na uchunguzi wake kwa wasichana wengine ambao wameweka picha zao katika mitandao hiyo wakijiuza, ambapo walipopigiwa simu walijibu na kufika katika maeneo waliyokubaliana.

Source: Mwananchi : www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1683124/-/item/1/-/sv9a9tz/-/index.html